Idara ya Kiswahili
Mwalimu Khamadi
Mkuu wa Idara
Idara ya Kiswahili
Naam, mbiu ya mgambo ikilia lazima kuna jambo. Katika shule ya mfinyanzi, tunafahamu fika kwamba mkono mmoja haumulei mwana, aidha umoja ni nguvu utengano ni udhaiffu. Hii ndio nguzo dhabiti ambayo hutuelekeza na kutuendeleza katika utekelezaji wa kazi idara yetu ya Kiswahili. Chambilecho kinga na kinga ndipo moto uwakapo, kila siku sisi hujitia shime jinsi ya
kukikuza na kukitukuza Kiswahili katika shule yetu tajika. Wanajopo hujikakamua kwa vyovyote vile kuhakikisha kwamba tumeyaafikia malengo yetu katika somo la Kiswahili. Walimu hutumia aina ainati kuhakikisha kwamba wanagenzi wote wana mtazamo chanya kuhusu lugha na somo la Kiswahili kwa kujieleza kwa ufusaha bila kutumia lugha mahuluti
au kiswakinge.Mshikamano wetu na vikao vya mara kwa mara na kutiliana pondo kumesaidia pakubwa lugha ya Kiswahili kukua na kufikia ufanisi kama ilivyodhihirika katika mtihani wa kitaifa mwaka wa 2021.
Hakuna mja yeyote anayefahamu kila kitu, hili limetusaidia sana kwani kila mara tunanoana na kujizatiti kujua mengi zaidi kwa kuulizana na kuelekezana pale ambapo hatuna ufahamu zaidi. Aghalabu sisi huhitimisha mtaala kwa walati unaofaa ili tuwe na muda mwafaka wa kudurusu na kutilia mlazo sehemu muhimu katika ufunzaji. Hili limesaidia sana kukua kwa lugha ya Kiswahili shuleni mwetu. Kumbuka, ubora na ubure wa adinasi yeyote umo ndani ya adinasi mwenyewe.
Tunakitukuza Kiswahili na si Kiswahili tu bali Kiswahili mufti, lugha mufti ni kioo mustaarabu na usuli wa heshima kwako na nafasi yako wewe mwenyewe. Naichukua fursa hii tenge na tengefu kuwapa mikono wa tahania wanajopo wote kwa kujitolea mhanga ili kuhakikisha kuwa Kiswahili kinapewa hadhi katika shule ya mfinyanzi. Aisee nani kama nyinyi ama kweli, wagombezi na wazalendo wa kupigiwa mfano sina cha kuwapa ila jalali azidi kuwajalia siha na rai njema daima dawamu aushini mwenu.